WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI AMEZINDUA RASMI VITUO VYA KUKUSANYIA MAZIWA VILIVYOJENGWA KWA UFADHILI WA BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO TANZANIA (TADB) KUPITIA MRADI WA TI3P



Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imezindua rasmi Vituo 23 vya Kukusanyia Maziwa (Milk Collection Centers – MCCs) vilivyojengwa na kuboreshwa kupitia Mradi  Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P).

Uzinduzi huo wa kitaifa umefanyika katika Kituo cha Kukusanyia Maziwa cha Nshamba (Nshamba MCC), Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, ukiongozwa na Mhe. Balozi Dkt.Bashiru Ally Kakurwa (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Waziri amesema mradi wa TI3P umeleta mageuzi makubwa katika mnyororo wa thamani wa maziwa nchini kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kupanua masoko kwa wafugaji wadogo, wa kati na wakubwa. Amesisitiza kuwa vituo vya kukusanyia maziwa si majengo tu, bali ni miundombinu ya kimkakati inayochochea mapinduzi ya kiuchumi kwa wafugaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ajira vijijini.

Mradi wa TI3P unaofadhiliwa na shirika la Gates Foundation na kutekelezwa na TADB kwa kushirikiana Mashirika Heifer International Tanzania na LandO’lakes Venture 37, ukiwa na lengo la kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji ili kukuza sekta ya maziwa kwa njia jumuishi na endelevu.

Mafanikio ya Mradi wa TI3P

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema hadi sasa mradi umewezesha:

Zaidi ya Shilingi bilioni 41 kutolewa kama mikopo kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa maziwa.

Ununuzi wa mitamba 3,254 yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.8 kwa lengo la kuongeza uzalishaji.

Ufadhili wa viwanda 15 vya usindikaji kwa Shilingi bilioni 22, na kuongeza uwezo wa kitaifa wa uchakataji wa maziwa.

Wafugaji 92,831 kufikiwa moja kwa moja kupitia huduma za kifedha, mafunzo na ugani.

Ruzuku fungamanifu (Matching Grants) ya Shilingi bilioni 1.448 kutolewa kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa.

Kuanzishwa na kuimarishwa kwa Vyama vya Wazalishaji  wa Maziwa (FPOs) 45 vinavyokusanya wastani wa lita 19,047 kwa siku.

Ujenzi na uboreshaji wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar, vyenye uwezo wa kukusanya lita 45,500 kwa siku na kuhudumia wafugaji 4,016 katika mikoa 8 na wilaya 18, kwa uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 1.157.

Ziara ya Ukaguzi – Kagera

Katika ziara yake mkoani Kagera, Mheshimiwa Waziri alitembelea Chama cha Ushirika cha Maruku, Bukoba Mjini, ambapo alishuhudia utekelezaji wa mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” unaolenga kuongeza kipato kwa vijana na wanawake kupitia ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa.



Kupitia chama hicho chenye wanachama 118 (asilimia 26 wanawake), wanachama 24 wamenufaika na mitamba 24 yenye mimba. Pia wamepata ruzuku ya Shilingi milioni 18 kupunguza marejesho ya mikopo, ukarabati wa MCC wenye thamani ya Shilingi milioni 10.4 pamoja na tanki la kuhifadhia maziwa la lita 2,000. Wanachama hao pia wamepatiwa mbegu bora za malisho aina ya Juncao na mafunzo ya ufugaji bora kutoka Heifer International.

Wafugaji wa Maruku wameunganishwa na soko la uhakika la Kahama Fresh Limited tangu Agosti 2023.

Katika Kituo cha Nshamba, chenye wanachama 541 (wanawake 83), TADB imewezesha uanzishwaji wa MCC yenye uwezo wa kukusanya lita 2,000 kwa siku pamoja na jenereta ya dharura. Wanachama 143 wako katika mchakato wa kunufaika na mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” kwa kupatiwa mitamba 45 yenye mimba.




Aidha, katika Ushirika wa UWAWAMA, Kayanga wilayani Karagwe, wanachama 76 wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa mitamba 110 yenye mimba na ruzuku ya Shilingi milioni 85 ya kupunguza marejesho ya mikopo.

Uwekezaji katika Usindikaji

TADB imeendelea kushirikiana na Kahama Fresh Limited tangu Oktoba 2021 kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda na ununuzi wa mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kusindika lita 20,000 za maziwa kwa siku, pamoja na magari maalum ya kukusanya na kusambaza maziwa.



Mwaka 2024, kupitia mpango wa "Kopa Ng'ombe, Lipa Maziwa", benki iliwezesha upatikanaji wa mitamba bora kutoka Kenya na Uganda. Mpango huo unalenga kuwasaidia wafugaji wadogo wadogo kupata ng'ombe wenye ubora kwa urahisi, ambapo wamekuwa wakipatiwa ng'ombe hao kwa mkopo wenye masharti nafuu.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji katika sekta ya mifugo, ikilenga kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kukuza ajira na kuinua kipato cha wananchi vijijini.

Bw. Nyabundege amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo na sekta binafsi utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha mafanikio ya TI3P yanaendelea kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.

Uzinduzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa kupitia mradi wa TI3P unaashiria hatua mpya katika mageuzi ya sekta ya maziwa nchini. Hatua hii inaweka msingi imara wa uchumi wa viwanda unaotegemea uzalishaji bora, thamani iliyoongezwa na ushiriki mpana wa wafugaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa.

Previous Post Next Post