| Baadhi ya viongozi toka Taasisi mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo TADB wameshiriki mkutano wa COP30 nchini Brazil |
BELÉM, BRAZIL Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeshiriki kikamilifu katika Mkutano wa 30 wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika hapa nchini Brazil, ikiwa kama mdau mkuu wa sekta ya kilimo nchini Tanzania. Ushiriki huu umetoa fursa muhimu ya kuonesha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia TADB, katika kukuza Kilimo Endelevu bila kuathiri mazingira, sambamba na kuendeleza azma ya matumizi ya Nishati Safi kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Moja ya vipaumbele muhimu vya Tanzania katika COP30 ilikuwa ni kusukuma mbele ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking). Tanzania inalenga kuhakikisha asilimia 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kilimo na Nishati Safi: Matumizi ya nishati chafu (kama vile kuni na mkaa) hupelekea ukataji miti kwa kiwango kikubwa, na hivyo kuathiri moja kwa moja ardhi inayotumika kwa kilimo na vyanzo vya maji.
Mchango wa TADB: TADB inatambua umuhimu wa nishati safi katika kulinda misitu na kuongeza tija ya kilimo. Benki inaangalia njia za kufadhili minyororo ya thamani ya mazao yanayohusiana na nishati safi, ikiwemo uendelezaji wa biofuels na nishati za mbadala zinazotokana na mazao ya kilimo (bioethanol na biogas).
Ushiriki wa TADB katika majadiliano ya 'Transforming Agriculture and Food Systems' na 'Stewarding Forests, Oceans, and Biodiversity' katika COP30, unasisitiza msimamo wa nchi kwamba Kilimo, Misitu, na Nishati Safi ni masuala yanayotegemeana na muhimu kwa Uchumi wa Kijani wa Tanzania.
Mkutano wa COP30 pia ulikuwa jukwaa la TADB kujenga na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa, benki za maendeleo, na wawekezaji binafsi. Lengo ni kuvutia rasilimali na teknolojia zinazohitajika kutekeleza mipango ya Kilimo-Hewa na Nishati Safi.
TADB inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maono ya Serikali ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, kuhakikisha inakuwa sekta yenye ushindani, tija, na inayojali mazingira.