TADB Yaendelea Kuimarisha Ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi


 Dodoma, 27 Januari 2026  Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa( Mb.) amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TABD) na kufanya mazungumzo  na yanayolenga kuendeleza ushirikiano kati ya wizara na benki hiyo  na kuitaka kuendeleza miradi ya sekta za mifugo na uvuvi.


Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Kambarage Tower kililenga kujitambulisha rasmi kwa uongozi mpya wa Wizara pamoja na kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati katika kufadhili miradi ya mifugo na uvuvi nchini.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru aliipongeza TADB kwa mchango wake katika kuunga mkono wafugaji na wavuvi, na kuitaka benki hiyo kupanua wigo wa utoaji wa mikopo nafuu kwa wafugaji wadogo ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hizo. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kushirikisha taasisi nyingine za kifedha kupitia TADB ili kuongeza upatikanaji wa mitaji kwenye sekta za mifugo na uvuvi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, alimpongeza Waziri kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kuahidi kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo, hususan kwa miradi inayowalenga vijana na wanawake kupitia programu mbalimbali za benki.

Bw. Nyabundege alieleza kuwa kama benki ya kisera, TADB imekuwa mshirika wa karibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo mikopo ya miradi ya boti za uvuvi, ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, pamoja na mikopo ya vijana kupitia Programu ya BBT Mifugo.

Alibainisha kuwa kupitia miradi ya boti na vizimba, TADB ilipokea jumla ya Shilingi bilioni 34.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, ambapo hadi sasa Shilingi bilioni 29.83 zimetolewa kwa wanufaika 5,932 katika mikoa 16 nchini. Kupitia miradi hiyo, jumla ya boti 219 na vizimba 536 vimetolewa kwa wanufaika.

Aidha, kupitia Mradi wa Vijana wa BBT Mifugo, TADB imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Shilingi milioni 847.3 kwa wanufaika 106 ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya mifugo.

Katika sekta ndogo ya maziwa, Bw. Nyabundege alieleza kuwa kupitia Mradi wa TI3P, TADB imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 40 kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa nchini. Kupitia mradi huo, benki hiyo pia imefanikiwa kujenga na kukarabati vituo 23 vya kukusanya maziwa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.1 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara, Halmashauri na wasindikaji wa maziwa.

Kupitia ushirikiano huo, TADB inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo endelevu ya sekta za mifugo na uvuvi kama nguzo muhimu za uchumi wa taifa.

Previous Post Next Post